Mmoja wa Wakufunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) akimwonyesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, moja ya vifaa vinavyotumiwa na abiria wakati meli inapozama wakati Naibu Waziri huyo alipohudhuria mahafali ya 12 ya chuo hicho, jijini Dar es Salaam
Mhandisi wa Meli kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Capt. Jumanne Karume. akimwelezea Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani namna meli inavyoendeshwa kwenye chumba cha nahodha, alipotembelea chuo hicho wakati wa mahafali ya 12 ya chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (kushoto), akiwatunuku wahitimu wa moja ya kozi zinazotolewa na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (kulia), akimkabidhi zawadi mwanafunzi aliyefanya vizuri katika mahafali ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya DMI, Bi. Rukia Shamte, wakiangalia zawadi aliyopewa mgeni rasmi na Chuo hicho katika mahafali ya chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, ameutaka uongozi wa Chuo cha Bahari cha Dar es salaam (DMI), kubuni na kutafuta vyanzo madhubuti vya mapato ili kusaidia kutatua changamoto zilizopo chuoni hapo.
Akizungumza katika Mahafali ya 12 ya Chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es salaam, Mhandisi Ngonyani amesema kuwa uwepo wa vyanzo imara vya mapato chuoni hapo utapelekea kutimiza malengo yake ya kutoa elimu na mafunzo yanayokubalika ndani na nje ya nchi.
“Wizara ingependa kuona DMI inaongeza ubunifu wa kutafuta vyanzo madhubuti vya mapato, Mkiwa na fedha mtaweza kutatua changamoto ndogo ndogo mlizonazo na kufikia malengo mliojiwekea”, amesema Mhandisi Ngonyani.
Ameutaka uongozi huo kukamilisha na kuwasilisha haraka upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mahitaji halisi ya majengo ya madarasa na ofisi za walimu ili kuiwezesha serikali kuchukua hatua stahiki.
Aidha, amewahakikishia wanafunzi kuwa Serikali itaendelea kusimamia mazoezi ya vitendo kwa wanafunzi wanaochukua fani mbalimbali chuoni hapo ili waweze kukubalika ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi chuoni hapo Bi Rukia Shamte, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kukamilisha taarifa ya Upembuzi yakinifu na kuiwasilisha kwake ili kuweza kufanyiwa kazi.
Ameiomba Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya chuo hicho ili kuboresha miundombinu ya chuo ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali vya mafunzo na ujenzi wa madarasa.
“ Kwa sasa tupo katika hatua ya mwisho za kumaliza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ujenzi wa jengo la wakufunzi pamoja na madarasa ili kukifanya chuo kibaki kwenye hadhi ya kimataifa, tukimaliza tutawasilisha serikalini kwa hatua zaidi, amesema Mwenyekiti wa Bodi
Zaidi ya wahitimu 70 wa fani mbalimbali wamehitimu katika mahafali ya 12 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano