.

.

Alhamisi, 8 Septemba 2016


Taasisi ya Misri yataka kuundwa kamati ya Kiislamu ya kusimamia Hija

Taasisi moja ya nchini Misri kwa jina la "Taasisi ya Uadilifu
na Ustawi wa Haki za Binadamu imezitaka nchi za Kiislamu
ziasisi kamati ya Kiislamu kwa ajili ya kusimamia masuala ya Hija.


Taasisi hiyo ya Uadilifu na Ustawi wa Haki za Binadamu yenye
makao yake nchini Misri imezitolea wito nchi zote za Kiislamu
khususan Iran, Pakistan, Afghanistan, Indonesia, Uturuki,
Chechniya na Misri yenyewe kuunda kamati kwa ajili ya kusimamia
masuala ya Hija na Umra. 

Taasisi hiyo imetoa ujumbe huo baada ya viongozi wa Saudi Arabia
kuwazuia Mahujaji wa Kiirani kushiriki katika ibada ya Hija ya mwaka huu.
Taasisi ya Uadilifu na Ustawi wa Haki za Binadamu ya Misri pia imesisitiza
katika ujumbe wake kuwa, nchi zote za Kiislamu zina haki ya kupanga
na kusimamia masuala ya ibada ya Hija. 

Hii ni kwa sababu al Kaaba haimilikiwi na Saudia na viongozi wa
nchi hiyo pekee, bali ni mali ya Waislamu wote wa dunia nzima.

Taasisi hiyo imeashiria kushindwa Saudi Arabia kudhamini
usalama na ulinzi wa mahujaji katika hija ya mwaka jana na
kusisitiza kuwa, kuwepo udhaifu katika kusimamia ibada hiyo
na kuwepo msongamano mkubwa wa mahujaji kupita kiasi
kulisababisha kuaga dunia mahujaji wengi wa Nyumba Tukufu
ya Mwenyezi Mungu. 

Taasisi ya Uadilifu na Ustawi wa Haki za Binadamu ya Misri
pia imeashiria shambulio la kigaidi la hivi karibuni karibu na
Masjidul Nabii na kueleza kuwa, viongozi wa Saudia hata
wameshindwa kuzuia kutekelezwa shambulio la kigaidi karibu
na msikiti huo huku wakiwatwisha Mahujaji masharti yasiyofaa
na kuyazuia mataifa mengine ya Kiislamu kushiriki katika
ibada ya Hija.